Breaking News

Wavulana huenda wakaruhusiwa kuvalia sketi shuleni London

 East Essex
Baadhi ya wavulana shule moja ya East Sussex walivalia sketi shuleni mwaka jana

Wavulana katika shule moja ya kibinafsi kaskazini mwa jiji la London huenda wakaruhusiwa kuvalia sketi iwapo sheria mpya kuhusu sare ya shule zitaidhinishwa.
Shule hiyo ya Highgate inapanga kuruhusu wanafunzi kuvalia sare yoyote ile ambayo wanataka bila kujali jinsia.

Wamechukua hatua hiyo baada ya kugundua watoto wengi wanauliza maswali kuhusu jinsia yao.
Shule hiyo, ambayo hutoza karo ya hadi £6,790 kwa kila muhula, pia inapanga kuvifanya vyoo kuwa huru kwa watoto wa jinsia zote.

Aidha, hakutakuwa na michezo tofauti ya wasichana na wavulana.
Wasichana katika shule hiyo kwa sasa huruhusiwa kuvalia sare ya wavulana - suruali za rangi ya kijivu, jaketi za rangi ya buluu iliyokolewa na tai.

Lakini wavulana hawaruhusiwi kuvalia sketi za rangi ya kijivu ambazo huvaliwa na wasichana pekee, lakini sasa wataruhusiwa sheria mpya kuhusu mavazi shuleni humo itakapopitishwa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Adam Pettitt amesema wazazi watashauriwa kabla ya mabadiliko hayo kuanza kutekelezwa.

Hata hivyo, amekiri kwamba kuna baadhi ya wanafunzi wa zamani wa shule hiyo ambao wameandika barua kulalamika kwamba shule hiyo inachukua mwelekeo usiofaa.
Makundi ya kutetea usawa wa jinsia shuleni yamelazimisha walimu kubadilisha, hata lugha wanayotumia kuwarejelea wanafunzi.

Aidha, misemo kama vile „kuwa mwanamume", haikubaliki tena.
Takwimu pia zinaonyesha idadi ya vijana wanaotaka kubadilisha jinsia yao inaongezeka.
Mwaka 2011, mvulana wa miaka 12 Chris Whitehead alivalia sketi na kwenda nayo shuleni baada ya kukerwa na sheria kuhusu sare katika shule ya Impington Village College, karibu na Cambridge.
Wanafunzi hawakuruhusiwa kuvalia kaptura wakati wa majira ya joto.

Mvulana huyo wa mwaka wa nane alisema alifanya utafiti na kugundua kwamba kulikuwa na upungufu katika sheria ya sare ya shule, na ndipo akaamua kuvalia sketi.

Mwaka uliopita, kundi la wavulana katika shule ya Longhill eneo la Rottingdean, East Sussex walivalia sketi kulalamikia adhabu waliyokuwa wamepewa kwa kuvalia kaptura shuleni siku ambayo ilikuwa na joto kali.

Source: BBC Swahili

No comments