Kivuko kipya Magogoni-Kigamboni chafanyiwa majaribio
Hatimaye
 kivuko kipya cha MV KAZI kimefanyiwa majaribio ya kubeba abiria na 
magari  kwa mara ya kwanza Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa 
matengenezo yake.
Majaribio
 hayo yalifanyika kulingana na sheria na taratibu za vyombo vya majini 
ambayo inavitaka vyombo vyote vya majini kufanyiwa majaribio kabla ya 
kuanza kazi ili viweze kupatiwa cheti cha ubora “Seaworthiness 
Certificate”.
Awali
 wataalam kutoka Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) waliweza  kupima 
ubora na uimara wa kivuko hicho kwa kutumia utaratibu wa kuweka mawe 
yenye kilo zinazolingana na uwezo wa kivuko pamoja na magunia ya mchanga
 ili kuweza kupima uwezo wa kivuko kulingana na mahitaji yaliyoainishwa 
kabla hakijabeba abiria na mizigo.
Zoezi
 hili pia lilihusu kufanyika kwa kipimo cha kuhakikisha kuwa kivuko 
hakilali upande mmoja yaani “Inclination test” ambapo kilionyesha Kivuko
 kiko sawa. Taarifa ya zoezi hili itakuwa sehemu ya vitu vya 
makabidhiano wakati wa upokeaji wa Kivuko.
Ujenzi
 wa MV KAZI umegharimu Shilingi Bilioni 7.3 za Kitanzania na kina uwezo 
wa kubeba abiria 800 magari 22 sawa na jumla ya tani 170. Kivuko hicho 
kitakabidhiwa rasmi hivi karibuni kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
 kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni Jijini 
Dar es salaam na kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo kufikia 
vitatu.
Kivuko
 cha MV KAZI kikiondoka kwa mara ya kwanza kutokea Magogoni kuelekea 
Kigamboni kikiwa na abiria na magari. Kivuko hicho kilikua kikifanyiwa 
majaribio mara baada ya ujenzi wake kukamilika kabla ya kukabidhiwa  kwa
 TEMESA.
Abiria
 wakiingia katika kivuko cha MV KAZI tayari kwa kuvuka kuelekea upande 
wa Kigamboni. Kivuko hicho kilikua kikifanyiwa majaribio ya kubeba 
abiria kwa mara ya kwanza baada ya ujenzi wake kukamilika hivi karibuni.
 Source: Mpekuzi 



No comments