MWANZA YAVUNJA REKODI YA MAUAJI YA WIVU WA MAPENZI
IKIWA ni siku chache baada ya mkazi wa
Mtaa wa Kanyerere jijini Mwanza, Maximilian Ndegere (40) Mwanza kumuua
mkewe Teddy Patrick (38) kwa risasi na kisha yeye kujiua, matukio ya
wanandoa kuuana kutokana na migogoro ya kifamilia na wivu wa kimapenzi
yameendelea kutokea jijini Mwanza.
Kutokana na mauaji hayo, Jeshi la Polisi
jijini Mwanza linamsaka kwa udi na uvumba mwanamume ambaye amemuua
mkewe kwa kile kinachoonekana kuwa ni wivu wa mapenzi na kisha kutokomea
kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ahmed Msangi alisema polisi
wanamtafuta Charles John (35) ambaye ni mkazi wa Pasiansi Mashariki
katika Kata ya Pasiansi, Manispaa ya Ilemela.
Kamanda Msangi alisema John alishiriki
katika tukio la kumpiga mkewe Ester Charles (30), Mei 30 mwaka huu saa
9.09 alfajiri na kumwacha akiwa amekufa chumbani kwake huku mwili ukiwa
na majeraha.
Alisema katika kipindi chote cha
mahusiano yao, wawili hao walikuwa kwenye migogoro ya mara kwa mara ya
kifamilia, ambayo mwanamke huyo alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.
Alisema siku hiyo ya ugomvi, majirani
walisikia ugomvi ukiendelea kati ya wanandoa hao, na walikwenda
kuwasuluhisha na kuwasaidia kwa vile walizoea kuwasikia wakipigana mara
kwa mara na kisha kuelewana na kuendelea na maisha yao kama kawaida.
“Baada ya muda kupita majirani
hawakusikia ugomvi tena, na kudhani kuwa wameelewana, lakini baadaye
alisikika mtoto mdogo akilia kwa muda mrefu ndipo majirani walikwenda
dirishani kuangalia na kumuona mama yake akiwa amelala kimya kitandani
bila ya kumsaidia mtoto, huku baba yake akiwa hayupo, walipata shaka na
kutoa taarifa polisi,” alifafanua Kamanda Msangi.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa
walikwenda kwenye eneo la tukio na kumkuta Ester akiwa tayari amekufa
huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kupigwa na kitu kizito. Aidha
shingo yake ilikuwa imekabwa na kitambaa kigumu.
“Baada ya mume, kuona mke wake amekufa,
huyu aliamua kukimbia kusikojulikana na sisi tumeanzisha msako mkali wa
kumtafuta na tutahakikisha tunamkamata,” alieleza.
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi
wa mauaji hayo ya kinyama na kuongeza kuwa mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi
na uchunguzi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa
ajili ya maziko.
Katika tukio jingine, Kamanda Msangi
alisema Melikiad Misana (50) ambaye ni mkazi wa Miriti wilayani Ukerewe
amekufa wakati akiwa njiani kukimbizwa hospitalini baada ya kuchomwa na
kitu chenye ncha kali mgongoni kwake upande wa kushoto na mkewe
Bukherehere William (25) ambaye naye alijeruhiwa na mumewe kwa kuchomwa
na kitu chenye ncha kali kwenye mikono yake, tumboni na kusababisha
utumbo kutoka nje baada ya kuzuka kwa ugomvi baina yao.
Kamanda Msangi alisema uhalifu huo
ulifanyika Mei 29, mwaka huu saa 4.15 asubuhi katika Kitongoji cha
Kamengo Kijiji cha Muriti Tarafa ya Ilangara wilayani Ukerewe, ambako
inadaiwa siku ya tukio, Bukherehere hakulala nyumbani kwake, lakini
baadaye alirudi nyumbani akiwa amelewa chakari kitendo ambacho
hakikumfurahisha mkewe.
“Kutokana na hali hiyo, wanandoa hao
walijikuta wakiingia kwenye ugomvi na kisha kuanza kupigana kwa kutumia
vitu vyenye ncha kali, huku kila mmoja akimchoma mwenzake hali
iliyosababisha wote kupoteza fahamu kutokana na majeraha waliyopata,”
alifafanua Kamanda Msangi.
Alisema baada ya majirani kupata
taarifa, walitoa taarifa polisi na polisi walipofika kwenye eneo la
tukio waliwachukua majeruhi na kuwakimbiza hospitalini, lakini wakiwa
njiani mwanamume alifariki dunia huku mkewe akiwa hajitambui.
Alisema majeruhi amelazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe akiendelea kupatiwa matibabu akiwa chini
ya ulinzi wa polisi huku polisi wakiendelea na upelelezi kuhusu mauaji
hayo. Alisema hali yake sio nzuri na mwili wa mumewe umehifadhiwa
hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi
.
IMEANDIKWA NA NASHON KENNEDY,-HABARILEO MWANZA
No comments