Magufuli: Majambazi lazima watakamatwa hawatapenya.
RAIS John Magufuli amesema kundi la
majambazi linaloendesha mauaji mkoani Pwani hasa katika wilaya za
Mkuranga na Kibiti halitapenya, bali litakamatwa kokote waliko.
Amesema
amani ni jambo la msingi katika uwekezaji na akawataka wananchi
kuwaambia ndugu zao ambao wanawafahamu kwamba wanafanya vitendo hivyo,
kuacha mara moja.
“Hawatapenya, vyombo
vya ulinzi na usalama viko imara, hapo walikuwa wanajaribu kupiga mruzi
tu,” alisema Rais Magufuli jana asubuhi alipozungumza na wananchi wa
Kijiji cha Mkiu Wilaya ya Mkuranga wakati wa kuweka jiwe la msingi la
Kiwanda cha Vigae cha Good Will.
Alisema nchi inahitaji amani ili wawekezaji waje kwa wingi, kuwekeza miradi mbalimbali.
Alisema
Mkoa wa Pwani umebadilika kutokana na viwanda vingi kujengwa mkoani
humo na kusaidia kupunguza tatizo la ajira. “Wilaya ya Mkuranga peke
yake ina viwanda 83, naambiwa Mkoa wa Pwani una viwanda zaidi ya 200,
haya ndio maendeleo tunayotaka, akitokea mtu anahatarisha uwekezaji huu
lazima tushughulike naye,” alisema Rais Magufuli.
Aliwahakikishia
wawekezaji wa kiwanda hicho cha GoodWill Tanzania Ceramic Co. Ltd kuwa
amani itakuwepo eneo hilo na wasifikirie kwenda kujenga viwanda vingine
nje ya Tanzania, bali waendelee kujenga viwanda vingine vingi katika
wilaya hiyo.
“Jengeni hapa viwanda
vingi, bahati nzuri sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
SADC, soko la ukanda huu ni kama watu milioni 500, hivyo kuna uhakika wa
soko la bidhaa zenu, hivyo jengeni viwanda vingi hadi huko baharini,”
alisema Rais Magufuli.
Kiwanda cha
Vigae cha Good- Will kinatumia gesi asilia na asilimia 95 ya malighafi
ya kiwanda hicho, inapatikana eneo hilo na asilimia tano tu ndio
inayoagizwa kutoka China.
Kina uwezo
wa kuajiri watu kati ya 1,000 na 1,500. Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli amesisitiza kwamba kama kuna wananchi wanasubiri chakula cha
bure kupelekewa na serikali, watakufa kwa njaa kwani hakuna vya bure
chini ya utawala wake.
“Hizi kauli
zilizokuwa zinatolewa huko nyuma eti hakuna mwananchi atakayekufa kwa
njaa, mimi siiungi mkono. Sasa nasema chini ya utawala wangu kuna watu
watakufa kwa njaa wasipofanya kazi. Lazima tuambiane ukweli,” alisema
Rais Magufuli.
No comments