Breaking News

Binti wa miaka 15 abakwa na vijana wanne Jijini Mwanza.

Binti wa miaka 15 abakwa na vijana wanne Jijini Mwanza.
Image result for rpc mwanza
Watu watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi huku mwingine mmoja akiendelea kutafutwa kwa tuhuma za kumbaka binti mmoja mwenye umri wa miaka 15 wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
 
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kwamba tukio hilo limetokea tarehe 21/05/2017 majira ya saa moja kamili jioni katika maeneo ya mamlaka ya pamba, kata ya Kirumba ambapo inadaiwa kuwa binti huyo ambaye pia ni mkazi wa Kirumba alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtuhumiwa aliyejulikana kwa jina moja la Phili na walipanga wakutane katika maeneo hayo.
 
Inasemekana kuwa binti huyo alikutana na mpenzi wake mahali hapo kisha walikwenda sehemu yenye jumba bovu kuzungumza, wakiwa kwenye eneo hilo ghafla walitokea vijana wengine watatu wakishirikiana na Phili na kuanza kumfanyia ukatili kwa kumbaka.
 
Inasemekana kuwa wakati wakiendelea na ukatili huo binti alipiga yowe akiomba msaada kutoka kwa wananchi, wananchi walifika eneo la tukio na kumuokoa binti na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Fredy Remigius kisha walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo.
 
Askari walifika katika eneo la tukio na kufanya msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine huku wakishirikiana na wananchi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili huku mmoja aliyekuwa na mahusiano ya kimapenzi na binti akifanikiwa kutoroka.
 
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Fredy Remigius miaka 20, mkazi wa Kitangiri, Jackson Joseph miaka 17, mkazi wa Mlimani B na Frank Haruni miaka 18.
 
Kamanda Msangi amesema mahojiano na watuhumiwa waliokamatwa yanaendelea na pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani na kwamba majeruhi aliyebakwa amepelekwa hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

No comments